Umoja wa Mataifa umelaani kutekwa nyara na kuondolewa kwa lazima humu nchini kwa kiongozi wa upinzani wa Uganda Kizza Besigye.
Msemaji wa Katibu Mkuu wa UN Antonio Gutteres, Stephane Dujarric, ametoa wito wa uchunguzi wa haraka kufanywa kuhusu utekaji wa Besigye na mwaniaji huyo wa zamani wa Urais kuwachiliwa mara moja na asasi za usalama za Uganda.
“Nimezungumza muda mfupi na mke wa Kizza Besigye na amenieleza yanayojiri. Tunasikitishwa na yaliyosibu kiongozi huyo wa Upinzani.” Amesema Stephane Dujarric.
“Ni sharti familia yake na mawakili wake wafahamishwe kuhusu hali yake na anakozuiliwa” Ameongeza Dujarric.
Kinara wa Chama cha Narc Kenya Martha Karua aliyekuwa mwenyeji wa Bessigye humu nchini amelaani matukio yanayozingira kutekwa kwake.
Besigye alikuwa humu nchini kwa mwaliko wa Karua kuhudhuria hafla ya kuzinduliwa kwa kitabu cha tawasifu ya Karua.
Bi Karua amelaumu Rais William Ruto kwa kuendeleza ukiukaji wa haki za msingi za raia wa humu nchini na wa nchi za kigeni.
“Utawala wa sasa umekiuka haki za raia wake na sasa umefika viwango vya kukiuka haki za wageni na raia wa mataifa mengine.” amesema Karua.
“Tunajua Rais Ruto anaona Katiba kama Kizingiti kwa mipango yake lakini ni sharti atambue kuwa katiba iliwekwa kuwa kizingiti kwa nguvu za anayeshikilia kiti cha Rais.” amesema Karua.
Serikali ya Kenya tayari imekana kuhusika katika utekaji nyara huku katibu katika wizara ya mahusiano ya kigeni Korir Sing’oei akisema idara ya polisi imeanzisha uchunuguzi katika kisa hicho.