Waziri wa Fedha John Mbadi amerai wakenya kumpa kipindi cha mwaka mmoja kufufua uchumi wa taifa.
Akizungumza wakati wa ziara ya Rais William Ruto katika eneo la Nyanza; mwenyekiti huyo wa zamani wa chama cha ODM amesema anashauriana na Rais kuhusu mikakati ya ufufuzi wa uchumi.
“Nitamshirikisha Rais William Ruto na tutafufua uchumi. Nataka kuwahakikishia Wakenya kuwa uchumi wa nchi utakuwa kwenye mkondo sahihi… nipe tu mwaka mmoja, na mwaka wa pili utaanza,” Mbadi amesema.
Matamshi ya Mbadi yanajiri wiki chache baada ya taifa kushuhudia misururu ya maandamano ya kizazi cha Gen-Z iliyochochewa na hali duni ya uchumi.
Kauli yake inakinzana na ya hapo awali iliyoonekana kukashifu Rais kwa kuomba muda Zaidi kutekeleza mageuzi ya uchumi.
Wakati wa ziara yake Rais Ruto amezindua miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa usambazaji maji Mjini Oyugis.
“ Tumetenga Zaidi ya shilingi milioni mbili kutekeleza mradi sawia na huu katika mji wa Kendubay na Homabay. Eneo hili lazima litaendelea kupata maendeleo chini ya utawala wangu,” amesema Rais.
Rais amepata mapokezi mema katika maeneo aliyoyazuru kinyume na alipokuwa akihasimiana na kinara wa Azimio Raila Odinga ambaye anaamika kuwa kigogo wa kisiasa wa Nyanza.