Chama cha Thirdway Alliance kimewasilisha kesi katika mahakama ya kikatiba kutaka rais Uhuru Kenyatta kulazimishwa kuufanyia kazi ushauri wa jaji mkuu David Maraga wa kulivunja bunge chini ya siku 21.
Kupitia wakili wake Elias Mutuma, chama hicho kinahoji kuwa ushauri huo wa Maraga ni sharti utekelezwe chini ya siku 21 na rais hafai kuupuza.
Chama hicho kwenye ombi lake vile vile kinataka ufafanuzi wa mahakama hiyo ya kikatiba kuhusu aina ya uchaguzi utakaoandaliwa iwapo bunge litavunjwa.
Kwa mujibu wa chama hicho, kuvunjiliwa kwa bunge kutasababisha kuandaliwa kwa uchaguzi mdogo katika kila eneo bunge na wala sio uchaguzi mkuu ambapo wabunge watakaochaguliwa watahudumu katika muhula wa miaka mitano.
Itakumbukwa kwamba jaji wa mahakama kuu Weldon Korir ametoa agizo linalomzuia rais kuufanyia kazi ushauri huo wa Maraga mpaka kesi iliyowasilishwa mahakamani na walalamishi wawili Leina Konchellah na Mohsen Abdul itakasikilizwa na zaidi ya jaji mmoja.