Mbunge wa Kapsaret Oscar Sudi ameondoa kesi ya uhalifu dhidi ya vijana kumi na sita wa kizazi cha Gen Z waliokua wameshtakiwa kwa madai ya kupora na kuharibu mali ya dhamani ya zaidi ya shilingi milioni mia moja hamsini katika eneo la burudani analo miliki jijini Eldoret.
Washtakiwa hao walikamatwa baada ya maandamano ya vijana wa Gen Z ya Juni mwaka wa 2024 yaliyoandaliwa kupinga mswada wa fedha wa mwaka wa 2024/25.
Hakimu mkuu wa mahakama ya Eldoret Cherono Kesse siku ya Jumatatu aliridhia ombi la Sudi la kuondoa kesi hiyo bila masharti akisisitiza kuwa kesi hiyo haiwezi kurejeshwa tena mahakamani.
“Kwa niaba ya wakurugenzi na baada ya kurejelea kauli za kila mshtakiwa aliyefikishwa mahakamani pamoja na kauli za mawakili wa pande zote kesi hii imeondolewa” Alisema hakimu.
Uamuzi huo wa mahakama unafuatia mkurugenzi Samuel Lemayan kumweleza Kesse kuwa aliagizwa na Sudi kuondoa kesi hiyo kwa sababu hakuwa na nia ya kuwaadhibu vijana hao.