Spika Wetangula awaadhibu wabunge waliopigana bungeni.

0

Spika wa bunge la Kitaifa Moses Wetangula amempiga marufuku ya siku tisini na kumzuia mbunge wa bunge la Afrika Mashariki (EALA) Falhada Iman kuingia katika majengo ya bunge.

Hatua hiyo inafuatia kisa cha Falhada kupigana na mbunge maalum Umulkher Harun Mohamed katika majengo ya bunge siku ya Jumanne.

Sawia spika Wetangula alimtaka mbunge huyo mteule wa zamani kuwasilisha kwa njia ya maandishi ombi la msamaha kwa bunge pamoja na tume ya huduma za bunge kufikia siku ya Jumatatu.

Wetangula alieleza kuwa mhusika alihitajika kutumia njia hiyo kwa sababu hakuwa mbunge aliyekuwa akihudumu kwa wakati huo.

“Mheshimiwa Falhada amepigwa marufuku ya kuingia katika majengo ya bunge kwa kipindi cha siku 90 kando na siku atakayokuwa akiwasilisha ombi lake la msamaha kwa spika, ambapo atasindikizwa na afisa wa usalama wa bunge,” Wetangula alitangaza.

Kwa kawaida tume ya huduma za bunge huwapa wabunge wa zamani pamoja na wabunge wa Afrika Mashariki fursa sawa na wenzao wanaohudumu ikiwemo kuzuru na kutumia vifaa vya bunge.

Umulkher kwa upande wake alilazimika kuomba radhi baada ya video iliyosambazwa katika mitandao ya kijamii kuwaonyesha wawili hao wakikabiliana kwa makonde.

Katika ombi lake la msamaha, Umulkher alisimulia matukio yaliyozingira kupigana kwao akiomwomba radhi Falhada, wabunge wenzake na wakenya kwa jumla.

Wetangula alilitaja tukio hilo kuwa la kusikitisha na lisilo mfaa kiongozi wa haiba ya mbunge sawia akitishia kumchukulia hatua mbunge aliyerekodi video hiyo.

Hatua ya spika ilijiri muda mfupi baada ya viongozi wanawake wakiongozwa na seneta mteule Veronicah Maina kukashifu vikali kisa hicho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here