SHIRIKISHO LA KRIKETI KENYA LAMSIMAMISHA KAZI MWEKA HAZINA KALPESH SOLANKI

0

Shirikisho la Kriketi nchini limemsimamisha kazi mweka hazina, Kalpesh Solanki, ili kuruhusu uchunguzi kuhusu usimamizi wa fedha za shirikisho hilo.

Katika taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Cricket Kenya Ronald Bukusi, shirikisho hilo lilisema kusimamishwa kwa Solanki kulianza tarehe 29 Agosti 2024.

“Kalpesh Solanki amesimamishwa kazi kama mweka hazina wa Cricket Kenya, kuanzia Alhamisi, Agosti 29, 2024,” taarifa hiyo ilisema. Kalpesh hata hivyo amesalia Kimya kuhusiana na swala hilo

Kufuatia azimio la Halmashauri Kuu ya Kriketi Kenya mnamo Jumatano, Agosti 28, 2024, Kamati Ndogo iliundwa ikiwajumuisha wanachama Pauline Njeru au Beryl Oyugi, Pearlyne Omamo, na Msajili wa Michezo au mtu aliyeteuliwa na afisi yake kwa mujibu wa taarifa.

Jukumu la kamati hiyo ni kuchunguza dosari yoyote katika hazina ya jezi kuanzia 2022 na usimamizi wa jumla wa fedha za Cricket Kenya.

Pia itatathmini usimamizi wa fedha na matumizi ya fedha za Cricket Kenya tangu bodi ya sasa ilipochukua hatamu hadi Agosti 28, 2024.Hii ni pamoja na kubaini ikiwa malipo yalifanywa kwa mujibu wa Katiba ya Kriketi ya Kenya, sera za usimamizi, maazimio ya bodi na masharti ya ufadhili yaliyowekwa na Baraza la Kimataifa la Kriketi.

Kamati hiyo inatarajiwa kuwasilisha ripoti ya kina ya matokeo yake katika mkutano mkuu ujao wa mwaka.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here