Tarehe 4 mwezi Februari kila mwaka huwa ni siku ya ulimwengu kuadhimisha siku ya saratani duniani mada kuu ikiwa ni kutoa hamasisho kuhusu aina tofauti za ugonjwa huu, jinsi ya kujikinga pamoja na upatikanaji wa matibabu.
Mwaka 2025 haijakuwa tofauti mashirika tofauti na waadhjiriwa wa ugonjwa huu wakijitokeza kuelezea kuhusu yanayokabiliana nayo inapofikia ni swala la saratani.
Hapoa nchini Kenya, kauli mbiu imekuwa ni kuhusu wagonjwa wanavyoadhirika kutokana na uhamisho wa bima ya afya kutoka NHIF hadi SHA ambapo wagonjwa wengi wamesalia kugharamikia huduma na matibabu kwa mpango wa SHA bado ungali unakumbwa na matatizo.
Mwenyekiti wa Muungano wa mashirika ya saratani nchini (KENCO) Elo Mapelu anataja hali si hali huku kiwango kinachogharamiwa na bima ya SHA kikiwa cha kiasi ikilinganisha na ada ya matibabu.
“SHA inagharamia malipo ya shilingi 300,000 kwa familia ilhali gharama ya matibabu kwa mtu mmoja ni Zaidi ya shilingi elfu mia tatu.” Amesema Mapelu.
Akiongeza, Mapelu amesisitiza haja ya gharama ya matibabu ya saratani kuangaziwa vilivyo ili kuhakikisha hakuna mgonjwa anarudi nyumbani kwa kukosa hela.
“Serikali inafaa kuweka mikakati ya kuwepo kwa hazina ya huduma za dharura kwa wagonjwa wa saratani baada ya kutumika kwa kiasi cha shilingi 300,000 chini ya SHA.” Mapelu amesema.
Kando na hayo, mwenyekiti wa shirika la waadhiriwa wa saratani nchini Priscah Githuka amepaza sauti ya kutaka kuongezwa kwa idadi ya wauguzi wanaowashughulikia wagonjwa wa saratani.
“Changamoto zipo ikiwemo pia ukosefu wa vifaa vya matibabu ya saratani.” Amesema Githuka ambaye aligunduliwa kuugua saratani mwaka wa 2014.
Ila si hayo tu, Githuka anadai licha ya kuongezeka kwa vituo vya saratani, baadhi yavyo havina dawa na kuwalazimu wagonjwa kusaka dawa kwingineko bila ya ufahamu wa iwapo dawa hizo ni halisi.
Kwa mujibu wa msimamizi wa mipango katika shirika la magonjwa yasiyo ya kuambukizwa (NCD Alliance) Gideon Ayodo asilimia 50 ya wagonjwa wanaolazwa hospitalini wanaugua magonjwa yasiyo yakuambukizana ikiwemo saratani.
Ayodo ametilia mkazo haja ya kila mmoja kuchukua hatua za kukabili saratani kwa kuzingatia maswala yanayozuia kugonjeka.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa shirika la waadhiriwa wa saratani nchini Priscah Githuka amerai umma kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu pindi wanapopatwa na dalili zinazoashiria saratani kama njia mojawapo ya kuidhibiti.