SERIKALI YASUKUMA AJENDA YA ODINGA KUWA MWENYEKITI WA AUC

0
Mkuu wa mawaziri Musalia Mudavadi pamoja na kinara wa Azimio Raila Odinga wakihudhuria kongamano la mawaziri wa jumuiya ya Afrika Mashariki Zanzibar.

Kamati ya kampeni ya kinara wa Azimio Raila Odinga ya kuwania uwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika inatarajiwa kuzinduliwa rasmi wiki hii.

Kamati hiyo itakayojumuisha viongozi wa Azimio na wale wa serikali itakuwa chini ya wizara ya mambo ya kigeni ikiendesha shughuli zake kutoka majengo ya Railways jijini Nairobi.

Serikali imeeleza kuunga mkono kikamilifu azma ya Odinga na hata kumfanyia kampeni kuhakikisha kwamba anatwaa ushindi.

Inaarifiwa kwamba Odinga anatarajiwa kuwasilisha stakabadhi zake za kuwania wadhifa huo wiki ya tatu ya mwezi huu wa Julai ambapo Kenya itakuwa imemteua rasmi kuwa mgombea wa wadhifa huo katika usimamizi wa bara la Afrika. 

Upande wake Odinga aliyekuwa waziri mkuu wa Kenya ameendeleza kampeni zake katika kongamano la mawaziri wa jumuiya ya  Afrika mashariki linaloendelea katika kisiwa cha Zanzibar.

Akihutubia kikao hicho Odinga amekariri nafasi kubwa ambayo Afrika inayo kujiimarisha kiuchumi,  kwa kutumia raslimali zake na kujitajirisha.

Pia ameendeleza mashinikizo ya kupanuliwa kwa mbinu za usafiri kupitia anga, barabara na bahari ili kufungua mipaka ambayo imewazuia waafrika kutangamana inavyostahili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here