Serikali yasema inajikakamua kuzuia mgomo wa wahudumu wa afya

0

Waziri wa Leba Simon Chelugui amewataka wahudumu wa afya kusitisha mgomo wao unaotazamiwa kuanza Jumatatu wiki ijayo ili kutoa nafasi kwa serikali kushughulikia malalamishi yao.

Chelugui katika taarifa anasema kwa sasa taifa linakabiliwa na mgogoro wa kiafya na halitakuwa jambo nzuri kwa wahudumu wa afya ambao huduma zao ni muhimu wakati huu kususia kazi.

Katika mojawapo ya njia za kuepuka mgomo huo, serikali imeliagiza shirika la kununua dawa na vifaa vya matibabu KEMSA kuachilia vifaa vyote vya kujikinga yaani PPEs ili kuwapa wahudumu wa afya kutumia.

Serikali za kaunti vile vile zimetakiwa kuharakisha utekelezwaji wa makubaliano yatakayohakikisha kuwa wahudumu wa afya wanapata bima ya matibabu kwa kutumia NHIF.

Waziri huyo anasema kamati ya pamoja imebuniwa kushiriki katika mazungumzo na wahusika wote katika juhudi za kutanzua mgomo huo utakaolemaza matibabu katika hospitali za umma.

Muungano wa madaktari KMPDU unasisitiza kuwa mgomo wao utaendelea iwapo serikali itakosa kutekeleza masharti yao ikiwemo kuwapa bima na vifaa vya kujikinga wanapokuwa kazini.

Muungano ya Wauguzi KNUN na ule wa Matabibu KUCO vile vile imetoa makataa kama hayo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here