Waziri wa usalama wa ndani Kithure Kindiki amedokeza serikali itatwaa sehemu ya msitu wa Shakahola kaunti ya Kilifi ambapo miili ya watu 429 imefukuliwa baada yao kuaga kutokana na kujifunga kula na kunywa.
Akizungumza mjini Kilifi, Kindiki ametaja mauaji hayo kama utovu wa usalama wa hali ya juu na kwamba serikali itajenga makavazi ya kumbukumbu eneo hilo.
Aidha waziri huyo wa usalama wa ndani amedokeza kuwa shamba hilo litatumika kuwazika baadhi ya watu ambao miili yao itakosa kuchukuliwa.
‘Serikali itachukua kwa lazma ekari elfu nne katika eneo la Chakama. Tutatumia sehemu hio kama makumbusho na kulaza walioaga katika maafa ya halaiki ya shakahola” Amesema Kindiki
Waziri Kindiki ametaja pia kuwa maafisa wa umma ambao walihusika vyovyote vile na mauaji hayo watakuwa wanachukuliwa hatua za kisheria.
Maafisa wa serikali ambao kwa njia moja au nyingine walihusika ama kukosa kuchukua hatua mpaka maisha ya wakenya ikapotezwa tutawachukulia hatua.” Amedokeza Kindiki.
Waziri huyo aidha amesisitiza kuwa washukiwa wakuu wakiongozwa na Mchungaji Paul Mackenzie watawajibikia maafa hayo.
“Wote ambao walisimamia vifo vya wakenya watajukumishwa na sharia wakongozwa na Mshukiwa mkuu(Paul Mackenzie) tutahakikisha kuwa haki imetendeka.” Amedokeza Kindiki
Watu 429 wanaripotiwa kushawishiwa na Mackenzie kufunga hadi kufa kwa Imani kuwa wataridhi ufalme wa mbingu.









