Muungano wa madaktari nchini (KMPDU) umesema hautakubali kutazama madaktari wakifariki kutokana na virusi vya corona wakiwa kazini kwa kukosa vifaa vya kujikinga dhidi ya virusi hivyo.
Katibu mkuu wa KMPDU Dr Chibanzi Mwachonda amesisitiza kuwa mgomo wao wa tarehe 6 Disemba ungalipo, iwapo serikali haitashughulikia matakwa yao 11 ikiwemo madaktari wote kupewa bima ya afya, vifaa vya kujikinga na corona na marupurupu ya kuhatarisha maisha yao kipindi hiki cha corona.
Mwachonda amemshtumu waziri wa afya Mutahi Kagwe kwa kudai kuwa baadhi ya madaktari wanapata ugonjwa huo wakiwa katika maeneo ya burudani na wala si kazini.
Muungano huo sasa unataka tume ya wahudumu wa afya kujumuishwa kwenye mswada wa marekebisho ya katiba mwaka 2020 kupitia kwa ripoti ya BBI.
Wakati uo huo…
Muungano wa wauguzi nchini KNUN umetoa ilani ya siku kumi na nne kushiriki mgomo wa kitaifa kulalamikia kupuuzwa na serikali kuu na zile za kaunti.
Katika notisi hiyo, katibu mkuu wa KNUN Seth Panyako anasema miongoni mwa masual wanayotaka yatatuliwe ni kucheleweshwa kwa mishahara yao, kwa mfano wanasema kaunti ya Vihiga haijawalipa mishahara kwa miezi kumi na nne.
Wauguzi hao pia wanataka kupewa bima ya afya ambayo itawasimamia kwa matibabu mbalimbali ikiwemo corona, kupewa vifaa vya kutosha kujikinga dhidi ya maambukizi ya corona wanapokuwa kazini na pia wenzao elfu saba waliohitimu kuajiriwa kazi ili wasaidie kukabiliana na janga la corona.
Panyako pia anaitaka serikali kufidia familia za wauguzi kumi na wanane ambao wamefariki hadi kufikia sasa baada ya kuambukizwa virusi vya corona wakiwa kazini.
Iwapo masuala hayo hayatashughulikiwa, wauguzi kote nchini wataanza mgomo wao tarehe saba Disemba, kujiunga na madaktari na maafisa wa kliniki ambao pia wametishia kugoma kuanzia tarehe sita Disemba.