Naibu rais William Ruto na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga wamekosoa kukamatwa kwa maseneta watatu wakati wa mjadala tata wa ugavi wa mapato katika serikali za kaunti.
Akikaribisha uamuzi wa kubuniwa kwa kamati ya maseneta kumi na wawili kutanzua kitendawili hicho, Ruto kupitia mtandao wake wa Twitter ameonya dhidi ya kuwatumia Polisi kuwatishia viongozi waliochaguliwa akisema hilo halifai na kwamba hiyo sio sababu iliyowafanya mamilioni ya Wakenya kuamka mapema na kupigia kura serikali ya Jubilee.
Odinga kwa upande wake amesema serikali haifai kutumia nguvu na badala yake kutafuta njia mbadala kutafuta mwafaka kuhusu mfumo utakaotumika kugawa pesa katika serikali za kaunti kwa njia sawa.
Ameonya kuwa iwapo swala hilo halitajadiliwa kwa njia ya hekima, taifa linakabiliwa na tishio la kugawanyika hata zaidi.