Naibu rais William Ruto amekaribisha hatua ya kinara wa chama cha ODM Raila Odinga kukubali kuongeza maoni zaidi kwenye ripoti ya BBI ili kujumuisha maoni ya watu kutoka jamii za wafugaji.
Ruto anasema hatua hiyo ambayo ni pamoja na kuruhusu maoni kutoka kwa wadau wengine wasioridhishwa na jinsi ripoti hiyo ilivyo kwa sasa itachangia pakubwa katika kuwa na mchakato usiokuwa na upinzani kabla ya kuandaliwa kwa kura ya maoni.
Kauli za Ruto zinawadia saa chache baada ya viongozi kutoka jamii za wafugaji wakiongozwa na waziri wa fedha Ukur Yattani kukutana na Odinga ambapo walisema wanaunga mkono ripoti hiyo.
Akizungumza baada ya kufanya kikao hicho, Odinga amekubaliana na viongozi hao kwamba jamii za wafugaji zimetengwa kwa muda mrefu na ni wakati wa kutafuta mbinu za kuwajumuisha kwenye masuala ya uongozi wa kitaifa.
Viongozi walioapa kuipinga ripoti hiyo awali, wameonekana kubadili msimamo wao, na sasa wanasema wanaunga ripoti hiyo vikamilifu na wanaamini kuwa masuala yao yatajumuishwa kwenye ripoti hiyo.