Rais William Ruto sasa anaitaka Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Humu Nchini (KRA) kukoma kutoa leseni kwa watu binafsi na mashirika yanayoagiza pombe kale almaarufu ‘spirits’ humu nchini.
Akizungumza mjini Kericho, Ruto amesema kuwa utawala wake utaipa kipaumbele vita dhidi ya pombe haramu ambayo imesababishwa maafa na kupoofika kwa mamia ya wakenya.
Rais amesema Mamlaka ya Ushuru nchini (KRA) inafaa kuwa katika mstari wa mbele kupigana vita dhidi ya pombe haramu.
“Hakuna leseni inatolewa kwa mtu ama watu wanaimport alcohol ama wanaleta mambo ya spirit ambayo inaharibu watoto wetu katika Kenya. Tumesema hio mambo ikome.”
Mkuu wa Nchi aidha amesihi wakenya kuahisi uraibu huo akihoji hakuna mtu anaeweza kupoteza maisha yake iwapo atakosa kunywa pombe
“Hakuna mtu atakufa kwa kukosa kunywa pombe na kama kuna mtu atakuwa mgonjwa tutapeleka hospitali for free,” amesema Rais.
Matamshi yake yanakuja siku moja baada ya Baraza la Mawaziri kupitisha mapendekezo 25 ya kukomesha matumizi uraibu wa pombe na dawa za kulevya nchini.
Mapendekezo hayo yalifuatia kifo cha takriban watu 20 huko Kirinyaga baada ya kunywa pombe inayodaiwa kuwa haramu katika eneo hilo huku wengine wakilazwa hospitalini.