Rais William Ruto ameahidi kuwanunulia sare za shule wanafunzi wote katika Shule ya Msingi ya Lenana iliyoko Dagoretti Kusini jijini Nairobi ambayo imefunguliwa asubuhi ya leo.
Akizungumza alipoongoza ufunguzi rasmi wa shule hiyo,Rais amebainisha kuwa wanafunzi wengi wametoka shule mbalimbali wakiwa na sare tofauti.
Ameagiza wanafunzi hao waruhusiwe kuendelea na masomo na sare za shule zao za awali wanaposubiria sare mpya.
“Kila mtoto ambaye atakuja hapa mara ya kwanza nitawanunulia uniform mpaka viatu. Hawa watoto wamekuja hapa na uniform za shule zingine, yule amekuja na nguo za nyumbani. Lakini hata kabla uniform haijafika hawa watoto waingie darasani waendelee kusoma,” Ruto amesema.
Rais aidha ameahidi kujenga zaidi ya madarasa 22 itakayotumiwa na wanafunzi wa darasa la kwanza hadi nane katika shule hiyo iliyojengwa kwenye ardhi ya shule ya Kitaifa ya Wavulana ya Lenana.
Ujenzi wa shule hiyo ulianza miaka minne iliyopita baada ya mkasa wa kuporomoka kwa shule ya kibinafsi ya Precious Talent na kusababisha kuaga dunia kwa wanafunzi 8 na kuwajeruhi wengine 64.
‘Tulikuja hapa mwaka wa 2020 baada ya ajali katika shule ya kibinafsi. Tuligundua kuna uhaba wa shule za umaa katika eneo hili ndipo tukaanza ujenzi huu. Sehemu iliyosalia nitahakikisha imekamilika.” Amesema Rais wakati wa uzinduzi huo.
Shule hjio inatarajiwa kukata kiu ya elimu ya watoto wa mitaa ya mabanda ya Ngando, Satellite, Dagoreti Corner, Deliverience na mitaa mingine.
Mkuu wa Nchi aliandamana na Mawaziri Kithure Kindiki (usalama wa Ndani) na Ezekiel Machogu (Elimu), Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja, Mbunge wa eneo hilo John Kiarie miongoni mwa viongozi wengine.