Wito wa Uwajibikaji kuhusu visa vya utekaji nyara na kutoroshwa kwa lazima kwa wakosoaji wa serikali unazidi kushika kasi; Shirika la Justice and Equality Council likiwa la hivi punde kutaka Inspekta Jenerali wa polisi Douglas Kanja na Mkurugenzi wa DCI Amin Mohammed kujiuzulu kutokana na visa hivyo.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, shirika hilo lenye makao yake nchini Uingereza limelaumu wakuu hao wa polisi kwa kushindwa kutekeleza wajibu wao wa kulinda raia kwa mujibu wa Katiba ya Kenya 2010.
Mwenyekiti wa Shirika hilo Sebastian Onyango amemtaka Rais William Ruto kuwawachisha kazi Kanja na Amin mara moja na kufanya mageuzi katika idara ya usalama humu nchini.
“Tunataka Inspekta jenerali wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi NPS na Mkurugenzi wa Idara ya upelelezi wa makosa ya Jinai DCI kufutwa kazi mara moja kwa kufeli kwenye jukumu lao la kulinda raia.” Amesema Onyango.
“ Rais William Ruto anapaswa kuchukua hatua za haraka kufanya mageuzi katika uongozi wa kikosi cha polisi,”ameongeza Onyango.
Onyango amesisitiza haja ya mageuzi makuu kwenye upeo wa uongozi wa polisi akisema ndio njia ya kipekee ya kurejesha imani ya Wakenya kwa idara hio.
“Tunataka Tume ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi NPSC kuanzisha mchakato wa kusaka washikilizi wa afisi za Inspekta Jenerali na Mkuu wa DCI na uchunguzi kuhusu utendakazi wa washikilizi wa sasa kuanzishwa.” Onyango amerai.
Maafisa wa polisi siku za hivi karibuni wamelaumiwa kwa kuteka nyara wakosoaji wa Rais William Ruto akiwemo mchora vibonzo Gideon Kibet almaarufu ‘Kibet Bull’ madai yaliyokanwa na Inspekta Jenerali Kanja.
Kanja kwenye taarifa kwa vyombo vya habari alisema maafisa wa polisi hawana ufahamu kuhusu wanaotekeleza utekaji nyara huo akiahidi uchunguzi wa kina katika visa hivyo.