Rais William Ruto amefanya mazungumzo na mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron kuhusu mzozo unaoendelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kabla ya mkutano wa dharura wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki hapo kesho.
Vyanzo vya habari likiwemo shirika la habari la AFP viliripoti kuwa takriban watu 17 wameuawa katika mapigano hayo na zaidi ya 300 kujeruhiwa.
Hatua hiyo imekuja baada ya waasi wa M-23 kutangaza kuwa wameuteka mji mkuu wa Goma mashariki mwa DRC, pamoja na tawi la Goma la shirika la utangazaji la serikali RTNC.
Ruto amebainisha kuwa Rais Macron alielezea kuunga mkono juhudi za kikanda kukabiliana na hali ambayo tayari ni tete katika eneo hilo.
“Rais Macron pia ameahidi kuunga mkono hatua zinazotekelezwa,,kwa ushiriki wa Kenya kusaka amani nchini Somalia, Sudan na Sudan Kusini,” Ruto amesema.
Kando na hayo, mkuu wa nchi alifanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio kuhusu masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujumbe wa Kenya nchini Haiti.
“Pia tulijadili ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Msaada wa Usalama wa Kimataifa (MSS) nchini Haiti na tukakubaliana juu ya mkakati wa pamoja wa kuhakikisha kuwa ujumbe huo unatimiza malengo yake,” inasomeka taarifa hiyo, kwa sehemu.
Mazungumzo na Rubio pia yalihusu Mkataba wa Ubia wa Kimkakati wa Biashara na Uwekezaji (STIP) ambao unalenga kuongeza uwekezaji, kukuza ukuaji wa uchumi endelevu na shirikishi.