RAIS RUTO ATUNUKU MAWAKILI 8 HADHI YA ‘SENIOR COUNSEL’

0

Rais William Ruto hii leo amewatunuku mawakili wanane na hadhi ya Wakili Mkuu almaarufu ‘senior counsel’ ambayo Ndio hadhi ya juu Zaidi katika taaluma ya uwakili humu nchini.

Hadhi hio hutwikwa kwa mawakili wenye tajriba ya juu baada ya kupendekezwa na kamati ya mawakili wakuu inayoundwa na chama cha mawakili humu nchini (LSK).

Miongoni mwa wale ambao sasa watajiunga na kundi la mawakili wakuu ni pamoja na aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK) Gichuhi Allen Waiyaki, pamoja na aliyekuwa mwenyekiti wa LSK Nairobi Charles Njiru Kanjama.

Wengine ni pamoja na McCourt Kevin Dermot, Mwaura Lillian Wakiiya, Gathenji Mbuthi, Kibet Jinaro Kipkemoi, Kamau Karori na Mutua Eric Kyalo

Baadhi ya mahitaji ya mtu kuhitimu kutunukiwa cheo cha senior counsel ni pamoja na kuwa mwanasheria ambaye anafunza na kukuza wanasheria wengine katika taaluma yao na hajapatikana na hatia ya utovu wa nidhamu wa kitaaluma na Kamati ya Nidhamu ya LSK.

Lazima awe mtu mwadilifu, mwenye mwenendo wa kitaaluma usio na doa na mwenye tabia njema ambaye amechangia maendeleo ya taaluma ya sheria kupitia maandishi na mawasilisho ya kitaaluma.

Baadhi ya mawakili tajika ambao wametunukiwa hadhi hio miaka ya nyuma ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Sheria na kiongozi wa chama cha NARC-Kenya Martha Karua, aliyekuwa Makamu wa Rais na kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na Philip Murgor.

Wengine ni pamoja na Jaji Mkuu Mstaafu Dkt. Willy Mutunga, aliyekuwa mkuu wa sheria Amos Wako, Ahmednasir Abdullahi, Nzamba Kitonga na waziri wa zamani wa Ulinzi Raychelle Omamo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here