Rais Ruto atia saini kuwa sheria mswada wa marekebisho ya IEBC

0
Rais William Ruto (katikati) akitia saini mswada wa marekebisho ya IEBC katika jumba la kimataifa la mikutano (KICC) jijini Nairobi.

Rais William Ruto ametia saini kuwa sharia mswada wa marekebisho ya tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC wa mwaka wa 2024.

Mswada huo ulikua miongoni mwa miswada tisa iliyotayarishwa kwa ajili ya kufanikisha utekelezwaji wa mapendekezo kwenye ripoti ya kamati ya kitaifa ya maridhiano (NADCO).

Sheria hiyo sasa inapendekeza kubuniwa kwa jopo la watu tisa litakalowateua makamishna wa tume hiyo ya uchaguzi.

Hii inafuatia kamati ya pamoja ya sheria katika bunge la kitaifa na seneti (JLAC) kupanua kamati ya uteuzi wa makamishna wa IEBC kutoka saba hadi wanachama tisa.

Kutiwa saini kwa mswada huo kunatazamiwa kumaliza mzozo wa kikatiba kutokana na pengo la uongozi lililokua likishuhudiwa katika tume hiyo.

Nafasi ya mwenyekiti, pia makamishna sita imesalia wazi mwaka mmoja baada ya mwenyekiti Wafula Chebukati na makamishna wawili kukamilisha muhula wao wa kuhudumu mwezi Januari mwa 2023.

Kustaafu kwa watatu hao waliokuwa wamesalia kulijiri baada ya wenzao wanne kujiuzulu baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Kulingana na hitaji la kikatiba, IEBC ilivyo kuwa haingeweza kuendesha majukumu yake yakiwemo kutayarisha na kuendesha uchaguzi wala kuchora mipaka ya maeneo-wakilishi pasi na idadi hitajika ya makamishna.

Hafla ya kutiwa saini kwa mswada huo ilifanyika Jumanne katika jumba la kimataifa la mikutano la KICC jijini Nairobi ambapo ilihudhuriwa na kinara wa upinzani Raila Odinga, viongozi wa kamati ya NADCO  wakiongozwa na Kalonzo Musyoka na kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Kimani Ichung’wa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here