Rais William ruto ameongoza taifa kuomboleza kuaga kwa wanafunzi 17 katika mkasa wa moto uliotokea usiku wa kuamkia leo katika shule ya Hillside- Endarasha kaunti ya Nyeri.
Kiongozi wa taifa kupitia ukurasa wake wa X ameahidi kuhakikisha waliohusika na kisa hicho kilichotokea mwendo wa saa tisa asubuhi wanaajibishwa.
“Mawazo yetu yako kwa familia za watoto waliopoteza maisha katika mkasa wa moto katika shule ya Hillside Endarasha Academy kaunti ya Nyeri.” Amesema kiongozi wa Taifa.
Rais aidha ameahidi kuwa Wizara ya Usalama wa Ndani itakusanya rasilimali kusaidia familia zilizoathirika na mkasa huo.
Ujumbe wa Rais umesisitizwa na Kinara wa Chama cha ODM Raila Odinga ambaye amewaombea stahamala waliothirika.
Naibu wa Rais Rigathi Gachagua kwa upande wake ametaka wasimamizi wa shule kuhakikisha mikakati inawekwa kuhakikisha usalama wa wanafunzi wakiwa shuleni.
“Tunaomba shule zitekeleze hatua za usalama na usalama kama ilivyoainishwa na Wizara ya Elimu na mashirika mengine ili kuzuia matukio kama haya.” Ameandika Gachagua katika akaunti yake X.
Waziri wa Elimu Julius Migosi amekatiza safari yake ya taifa la Uchina kutokana na kisa hicho na anatarajiwa kurejea humu nchini leo hii.
Wengine ambao wametuma risala zao za rambirambi ni Pamoja na Spika wa bunge la kitaifa Moses Wetangula, Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru, Waziri wa Michezo Kipchumba Murkomen na mbunge Didmus Barasa.