Rais William Ruto amempongeza John Dramani Mahama kwa kuchaguliwa tena kama Rais wa Jamhuri ya Ghana.
Mahama aliibuka na ushindi wa asilimia 56.6 dhidi ya asilimia 41.3 Naibu wa Rais Mahamudu Bawumia aliyewania kwa tikiti ya chama tawala cha New Patriotic Party (NPP).
Rais wa sasa NANA Akufo- Addo alifungiwa nje ya uchaguzi huo baada ya kuhudumu mihula miwili kama kiongozi wa taifa hilo la Afrika magharibi.
“Kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Kenya na kwa niaba yangu binafsi, nawasilisha kwa kupitia kwako kwa Serikali na Wananchi wa Jamhuri ya Ghana pongezi zangu za dhati kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Ghana kwa mafanikio.” Amesema Rais Kwenye akaunti yake ya X.
Rais mteule alihudumu kama Rais kati ya mwaka wa 2012- 2017 alipopoteza kwa Nana Akufo – Addo.
Hata hivyo, hatamu ya mwisho ya Addo ilishuhudia kipindi kigumu zaidi kwa uchumi wa taifa hilo likishindwa kulipa madeni yake.
Rais William Ruto kwenye ujumbe wake amesisitiza uhusiano mwema baina ya Kenya na Ghana akiahidi kuendeleza uhusiano huo chini ya utawala wa Mahama.
“Mataifa yetu yana urafiki wa muda mrefu na kujitolea kwa ushirikiano wa kikanda na ustawi wa pande zote.” Ameongeza Rais kwenye ujumbe wake wa heri.
“Kwa hakika, ni nia yangu kuongeza na kuimarisha zaidi ushirikiano huu katika maeneo yenye maslahi kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya watu na mataifa yetu.”
Dramani Mahama ambae aliibuka na ushindi katika uchaguzi ulioandaliwa wiki jana Anatarajiwa kuapishwa rasmi Januari 7, 2025.