RAIS RUTO AAHIDI NAFASI ZA AJIRA; UBORESHAJI WA ELIMU KWENYE ZIARA YAKE YA NAIROBI

0

Rais William Ruto ameendeleza ziara yake katika kaunti ya Nairobi hii leo akizindua ujenzi wa madarasa katika shule ya wasichana ya st. Theresa’s iliyoko katika eneo Bunge la Mathare.

Kiongozi wa taifa ameahidi kufadhili ujenzi wa mabweni, madarasa na maabara Zaidi katika shule hiyo.

“Nimetoa shilingi milioni 5 kufadhili ujenzi wa bweni na maabara katika shule hii” amesema kiongozi wa Taifa.

Rais aidha ametumia fursa hiyo kusifia juhudi zilizochukuliwa na utawala wake kuboresha sekta ya elimu humu nchini.

Amesema mpango wa kuajiri walimu utaendelezwa ili kupunguza uhaba wa walimu katika shule za msingi, sekondari msingi na shule za upili.

“Munajua tuko na mpango wa kuajiri walimu. Mpango huo utaendelea ili kuhakikisha wanafunzi wa Mathare hawakosi elimu,” Rais amedokeza.

Rais Ruto aidha ameahidi kuongeza idadi ya vijana wanaofanya kazi katika mpango wa ‘Climateworks’ ambao amesifia kama uliowezesha uzalishaji wa nafasi za ajira.

“Nimesikia wito wa vijana wa Mathare wameniambia wanataka kujumuishwa kwenye Climateworks na nimeagiza gavana Johnson Sakaja kuhakikisha idadi hiyo inaongezwa ili vijana wapate ajira.” Rais amesema.
Kiongozi wa taifa ameandamana na wandani wake kwenye ziara hiyo kama Vile naibu wake Kithure Kindiki na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja.

Ziara hiyo ni ya kwanza tangu rais atie saini makubaliano na kinara wa upinzani Raila Odinga.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here