Rais Kenyatta yuko Ufaransa kwa ziara rasmi ya serikali

0

Rais Uhuru Kenyatta yuko nchini Ufaransa kwa ziara rasmi ya serikali ambapo tayari ametia saini mikataba mitatu ya makubaliano na mwenyeji wake Rais Emmanuel Macron.

Miongoni mwa makubaliano hayo ni ushirikiano wa serikali na mashirika ya kibinafsi ambapo mamlaka ya barabara kuu nchini KENHA imetia saini mkataba na kampuni ya Ufaransa ya Vinci Concessions kujenga barabara kuu ya Nairobi kuelekea Mau Summit kupitia Nakuru.

Mikataba mingine inahusisha ujenzi wa reli kutoka katikati mwa jiji la Nairobi hadi uwanja wa kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta na pia usambazaji wa nguvu za umeme zenye wati 400KV kutoka Menengai hadi Rongai.

Rais Kenyatta aliwasili Paris, Ufaransa jana jioni akiwa ameandamana na mawaziri Raychell Omamo wa masuala ya kigeni, Ukur Yattani wa fedha, James Macharia wa uchukuzi na Betty Maina wa biashara.

Balozi wa Kenya nchini humo Profesa Judi Wakhungu anasema ziara ya Kenyatta inalenga kuimarisha uhusiano baina ya Kenya na Ufaransa huku akidokeza kuwa zaidi ya  kampuni mia moja za Ufaransa zinahudumu nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here