Kwa mara ya kwanza rais Uhuru Kenyatta amezungumzia mswada tata wa ugavi wa mapato uliobua mgogoro katika bunge la Senate.
Akizungumza wakati wa kutoa vyeti kwa wakaazi wa Embakasi katika jumba la mikutano la KICC, rais Kenyatta amekanusha madai ya kuingilia mjadala huo na kusisitiza kuwa mamlaka ya mapato nchini CRA ndio ilipendekeza mfumo unaofaa kutumika kugawa pesa kwenye serikali za kaunti.
Rais Kenyatta vile vile amesema lengo la kuu ni kuwahudumia Wakenya na wala sio kujihusisha na siasa zisizokuwa na msingi.
Matamshi ya rais kuhusu mswada huo wa ugavi wa mapato yanawadia huku kamati ya maseneta kumi na wawili iliyobuniwa kutanzua mgogoro huo ikitazamiwa kuwasilisha bungeni ripoti yake Jumatatu wiki ijayo.