
Hutahitajika kutozwa chochote ili kupata kitambulisho cha kitaifa baada ya ada iliyokuwepo kuondolewa na kufanya huduma hiyo kuwa bure mara moja.
Hii ni kufuatia amri iliyotolewa na rais William Ruto siku ya Alhamisi akiwa kwenye ziara ya maendeleo katika kaunti ya Nairobi.
Amri hii inafutilia mbali agizo la awali la mwaka wa 2024 lililochapishwa katika gazeti rasmi la serikali kupitia wizara ya usalama wa ndani ambalo lilikuwa linatoza ada ya kupokea stakabadhi hiyo kwa mara ya kwanza kwa wanaohitimu umri wa miaka kumi na minane kutoka shilingi 100 hadi 300.
Rais William Ruto akizungumza huko Kibera, alitangaza kundolewa kwa ada hiyo akisema kuwa ni hatua ya kuwawezesha wakenya wengi iwezekanavyo kupata kitambulisho kwa urahisi.
Kiongozi wa taifa ametaja hapafai kuwa na ubaguzi inapofikia kuhusu swala la kitambulisho na kila mkenya ana haki ya kupewa stakabadhi hiyo muhimu.
“Mimi nataka nitangaze nikiwa hapa Kibra leo, ya kwamba kitambulisho kitolewe bila malipo yoyote na kwa mpango ambao hauna ubaguzi kwa wakenya.” Rais Ruto aliamuru.
“Mimi nimesema, maneno ya ubaguzi kwa mambo ya ID tuitolee mbali, kila mwananchi apatiwe kitambulisho,” aliongeza rais.
Tangazo hilo la kiongozi wa taifa linafuatia kilio cha umma hususan kutoka kwa vijana wanaofikisha umri wa miaka kumi na minane kuhusu ugumu wa kupata ada iliyohitajika kufanikisha shughuli hiyo.
Sawia, amri hiyo ya rais inajiri siku chache baada yake kuondoa hitaji la msasa kwa wakazi wa eneo la Kaskazini Mashariki mwa taifa wakati wa kutafuta vitambulisho