Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga ametofautiana na msimamo wa tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC kwamba maandalizi ya kurekebisha katiba kupitia kura ya maamuzi yatagharimu Sh14b.
Odinga katika taarifa ameisuta IEBC akidai kuwa kiwango hicho cha pesa ni njama ya tume hiyo kuiba pesa za mlipa ushuru.
Badala yake Odinga ameshikilia kuwa ni shilingi bilioni mbili pekee ndizo zinahitajika kuandaa kura hiyo ya maamuzi.
Kiongozi huyo wa chama cha ODM katika maelezo yake ametaja kuwa taifa hili liko na uwezo wa kutumia kiasi hicho kidogo cha pesa kuandaa kura hiyo ya kurekebisha katiba kutokana na miundo mbinu bora iliyopo ikiwemo barabara zitakazofanikisha usafirishaji wa vifaa vya kupigia kura.
Odinga alikuwa anajibu matamshi ya kaimu afisa mkuu mtendaji wa IEBC Hussein Marjian aliyewaambia wabunge kwamba wanakadiria kutumia kima Shilingi bilioni kumi na nne kuandaa kura hiyo kwa kuzingatia idadi ya wapiga kura ambayo ni milioni kumi na tisa.
Tayari rais Uhuru Kenyatta ametia saini mswada unaotoa nafasi ya kuanza kwa mchakato wa kujaza nafasi za makamishna waliojiuzulu.