Mahakama kuu imekataa kutoa agizo la kuzuia kuwasilishwa na kujadiliwa kwa hoja ya kumuondkoa naibu rais Rigathi Gachagua mamlakani katika bunge la seneti.
Katika uamuzi wake, jaji Chacha Mwita amesisitiza umuhimu wa ugavi wa mamlaka akitaja idara ya mahakama haifai kuingilia mchakato wa bunge.
Hata hivyo jaji Mwita amedokeza naiu rais ameibua maswala kadhaa yanayoangazia utaratibu wa kisheria na hivyo kutaka kesi hiyo kuwasilishwa kwa jaji mkuu Martha Koome kwa mwelekeo zaidi.
Amesema jaji mkuu anaweza kubuni jopo la majaji kusikiliza kesi hiyo na kuangazia kikamilifu maswala ambayo yameibuliwa na Gachagua.
Naibu Rais ambaye hadi kufikia sasa amewasilisha kesi 26 mahakamani kupinga kung’atuliwa kwake anatarajiwa kujitetea mbele ya bunge la seneti Jumatano baada ya wabunge 282 kuidhinisha mashtaka 11 dhidi yake.
Kati ya mashtaka kumi na moja yanayomkabili naibu wa rais ni Pamoja na kueneza ukabila na siasa za kieneo, tuhuma za kukiuka kifungu cha kumi cha katiba kuhusu maadili ya kitaifa na kanuni za utawala na kujipatia mali kwa njia isiyoeleweka.
Kulingana na Katiba, Gachagua ataondolewa moja kwa moja madarakani endapo mabaraua yote mawili yataunga mkono hoja dhidi yake, ingawa Gachagua anaweza kupinga hatua hiyo mahakamani – jambo ambalo amesema atafanya.
Seneti inahitaji wingi wa theluthi mbili ili kupitisha hoja ya kumng’oa madarakani Gachagua na iwapo itapitishwa itakuwa ni mara ya kwanza kwa naibu wa rais aliye madarakani kutiwa hatiani nchini.
Rais William Ruto hajatoa maoni rasmi kuhusu kumng’oa madarakani naibu wake, lakini amekuwa na rekodi katika siku za mwanzo za urais wake akisema hatamdhihaki makamu wake hadharani, akirejelea uhusiano mgumu aliokuwa nao na mtangulizi wake, Uhuru Kenyatta, wakati wa muhula wao wa pili wa ofisi.