Prof.Olive Mugenda amejiuzulu kama mwenyekiti wa bodi ya Hospitali ya Mafunzo , Rufaa na Utafiti ya Chuo Kikuu cha Kenyatta.
Pamekuwa na shinikizo kutoka kwa madaktari na wahudumu wengine katika taasisi hiyo ya kuondoka kwa Mugenda na Bodi yake kufuatia mgogoro wa uongozi kwenye taasisi hiyo.
Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wa Ikulu Hussein Mohammed, Rais William Ruto amekubali kujiuzulu kwa Mugenda.
“”Rais William Ruto amepokea na kukubali kujiuzulu kwa Profesa Olive Mugenda kama Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya Kufundisha, Rufaa na Utafiti ya Chuo Kikuu cha Kenyatta (KUTRRH), mara moja,” alisema Mohammed.
Wito wa Wafanyikazi uliotiwa saini na wawakilishi kutoka Muungano wa Madaktari (KMPDU) na ule wa Wauguzi (KNUN) ulieleza matakwa 10 kutoka kwa wafanyikazi wa matibabu na wasio wa matibabu katika taasisi hiyo kabla ya kuanza kufanya kazi.
Miongoni mwa mengine wafanyikazi hao walitaka Mugenda kuondoka kwa kuingilia usimamizi wa kila siku wa KUTRRH.
Afisa mkuu Mtendaji wa Hospitali hiyo Ahmed Dagane pia ameagizwa kuenda katika likizo ya muda usiojulikana.
Dk Zainab Gura ameteuliwa kuchukua nafasi yake katika nafasi ya kukaimu huku Isaac Kamau ambaye hivi majuzi aliteuliwa na Bodi kama kaimu afisa mkuu Mtendaji akirudishwa katika makao makuu ya wizara ya Afya.