Gavana wa Migori Zachary Okoth Obado anamtaka mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma kumpunguzia mashtaka kwenye kesi inayohusiana na ufujaji wa Sh73.4M.
Obado anakabiliwa na mashtaka Ishirini na mbili kati ya Ishirini na saba kwenye kesi ambapo ameshtakiwa pamoja na watoto wake wanne.
Kwenye ombi lake kwa hakimu wa mahakama ya kupambana na ufisadi Lawrence Mugambi, Obado kupitia kwa wakili wake Kioko Kilukumi anaitaka mahakama kumlazimisha mkurugenzi wa mashtaka kupunguza mashtaka hayo na kufikia kumi na mbili kabla ya kuendelea kwa kesi hiyo.
Kilukumi ameiambia mahakama hiyo kwamba kumshtaki mteji wake na mashtaka Ishirini na mbili haitakuwa sawa kwani sio haki.
Obado ambaye aliachiliwa kwa dhamana ya Sh8M anakabiliwa na mashtaka mbalimbali ikiwemo ulanguzi wa pesa na kuiba pesa za umma.