Mbunge wa Alego Usonga Samuel Atandi amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya Bajeti katika bunge la kitaifa akichukua nafasi ya mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro.
Katika mabadiliko yanayoonekana kusukuma nje wandani wa naibu wa rais wa zamani Rigathi Gachagua mbunge wa Endebes Robert Pukose ameteulwia kuwa naibu wa mwenyekiti wa kamati hiyo.
Kwa mujibu wa ofisi ya karani wa Bunge Samuel Njoroge ni Atandi pekee aliyekuwa amewasilisha ombi la kujaza nafasi hiyo kufikia siku ya Jumanne kulingana na kanuni za bunge huku Pukose aliyekuwa awali akiongoza kamati ya afya akiwasilisha ombi kuwa naibu mwenyekiti wa kamati hiyo.
Atandi aliahidi kuhakikisha kuwa kamati ya Bajeti chini ya uongozi wake inatimiza majukumu yake ipasavyo.
“Tunataka kusema kuwa tunaenda kuhakikisha kuwa tunatimiza matarajio ya kamati hii, kamati ya bajeti ni kamati muhimu sana nguzo katika uwepo wa bunge. Kama mjuavyo bunge lina majukumu matatu pekee, utungaji wa sharia, uundaji wa bajeti na uangalizi” alisema Atandi
Katika mabadiliko mengine yaliyofanyika siku ya Jumatano kwenye kamati mbalimbali za bunge, mbunge wa Butere Tindi Mwale alichaguliwa kuongoza kamati ya Uhasibu (PAC).
Tindi alimshinda mbunge wa Rarieda Otiende Amolo katika kinyang’anyiro kilichovutia wawaniaji wawili pekee.
Mwakilishi wa kike wa Garissa Amina Udgoon Siyad alichaguliwa kuwa naibu mwenyekiti wa kamati hiyo chini ya Mwale.
Wengine waliokabidhiwa uongozi wa kamati mbalimbali za bunge ni pamoja na mbunge wa Runyenjes Erick karemba aliyechaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa kamati inayoangazia utekelezwaji wa katiba kuchukua nafasi iliyoshikiliwa na mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba.
Mabadiliko hayo ya uongozi katika bungeni yanaonekana kutoa nafasi zaidi kwa chama cha ODM kufuatia kurasmishwa kwa ndoa ya kisiasa baina ya rais William Ruto na kinara wa chama hicho Raila Odinga.