NUSU YA WAKAAZI WA NAIROBI HAWANA AJIRA – UTAFITI

0

Zaidi ya nusu ya wakaazi wa Nairobi na haswa wanaoishi kwenye vitongoji duni hawana ajira kutokana na janga la COVID19.

Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na shirika la utafiti la TIFA umebaini kuwa asilimia 54 ya wakaazi wa Nairobi walipoteza ajira au walikuwa na biashara yao na ikaanguka kufuatia janga hilo.

Asilimia 69 wanasema mapato yao yamepungua huku asilimia 43 wakisema hawapati tena mapato yao kutoka mahali walikuwa wanategemea.

Ili kukabiliana na hali hiyo, utafiti huo unasema asilimia 94 ya wakaazi wa Nairobi wamepunguza matumizi yao haswa kwa chakula na vinywaji.

Asilimia 42 ya wakaazi wa jiji wanahofia kuwa huenda wakakumbwa na baa la njaa iwapo janga la corona litaendelea kwa zaidi ya miezi mitatu ijayo.

Ni asilimia sita pekee ya wakaazi wa jiji waliohojiwa ambao wanasema kuwa wanaweza kuwekeza pesa zao.

Utafiti huu ulifanywa kati ya tarehe mbili na kumi na tano mwezi huu katika mitaa ya Huruma, Kibera, Mathare, Korogocho, Mukuru kwa Njenga na Kawangware ambapo watu 579 walihojiwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here