Aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya mawasiliano katika ofisi ya Waziri Mwenye mamlaka Makuu na mtangazaji tajika Salim Swaleh sasa anaomba msamaha kutokana na sakata ya ufisadi inayomkabili.
Katika kanda ya video iliyofikia meza ya Shajara ; Swaleh akionekana kuzidiwa na hisia; amesema kwamba anasikitika kuvunja Imani ambayo bosi wake Musalia Mudavadi alikuwa nayo kwake.
Swaleh ambae hadi kuteuliwa katika afisi ya Mudavadi alikuwa mtangazaji wa habari kwenye televisheni ameelezea kupitia masaibu mikononi mwa maafisa wa polisi na waendesa mashtaka wanaotaka hongo kutoka kwake kwa dhana kuwa anafedha nyingi.
“ Mheshimiwa, umekuwa baba yangu kwa muda mrefu zaidi ambao nimekujua. Tumejenga uaminifu usio na kifani kati yetu na kwa muda wa moja na nusu uliopita nimekutumikia, nimetumikia ofisi yako nzuri, na kukutumikia kwa bidii isiyo na kifani.”
“ Nilivunja uaminifu na ninasikitika sana kuhusu hilo. Hakika nimejuta kuhusu hilo,” Amesema kwenye video hiyo.
Mwanahabari huyo ameelezea kupitia changamoto ya kisaikolojia akisema amefika kiwango cha kuwazia kujiangamiza.
“Ni mwisho wa mwezi, bili zinarundikana, mishahara imesimamishwa ghafla, nina mikopo, tafadhali tafuta moyoni mwako nafasi ya kunisamehe,” amesema.
Swaleh na wengine walitiwa mbaroni miezi kadhaa iliyopita kwa madai ya kuendesha mtandao wa ulaghai katika afisi ya waziri mwenye mamlaka makuu.
Wanadaiwa kuitisha kampuni moja hongo ya Zaidi ya dola 45,000 kwa kisingizio cha kuisaidia kampuni hio kupata kandarasi ya ujenzi wa uwanja wa michezo.