Tanzania imeondoa marufuku ya ndege za Kenya kuingia nchini humo saa chache baada serikali kusema raia wa taifa hilo jirani wanaowasili nchini hawatalazimika kujitenga.
Katika taarifa, mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya safari za angani nchini Tanzania TCAA Hamza Johari anasema ndege za Kenya sasa ziko huru kutumia anga yake na hata kutua katika viwanja mbalimbali vya ndege nchini humo.
Mashirika ya ndege ambayo sasa yana kibali cha kufanya ziara ya moja kwa moja kuingia na kutoka nchini Tanzania ni pamoja na KQ, Safari Link, FLY540 na Air Kenya Express.
Hatua hii inajiri saa chache baada ya mamlaka ya safari za angani nchini KCAA kutoa orodha mpya ya mataifa 147 ambayo raia wake wanaowasili nchini hawatajitenga kwa muda wa siku kumi na nne kutokana na hofu ya maambukizi ya virusi vya corona.
Hatua ya Kenya kuwalazimu watanzania wanaowasili nchini kujitenga ilionekana kuibua mzozo wa kidiplomasi baina ya mataifa hayo mawili na kusababaisha Tanzania kupiga marufuku ndege za Kenya kwenye anga zake.
Mataifa haya mawili yamekosa kuelewana kuhusiana na masharti ya kupambana na virusi vya corona huku Rais John Pombe Magufuli akitangaza kuwa Tanzania haina tena virusi vya corona.