Ndege iliyokuwa imsafirishe waziri wa afya Mutahi Kagwe hadi Nairobi kutoka Kericho imekumbwa na hitilafu za kimitambo.
Inaarifiwa kuwa waziri Kagwe alilazimika kushuka kwenye ndege hiyo baada ya juhudi za rubani kuiwasha kuambulia patupu.
Ndege hiyo aina ya 5Y-PKI ilikuwa imsafirishe waziri Kagwe pamoja na mkurugenzi wa huduma za matibabu katika wizara hiyo Dkt. Patrick Amoth.
Imemlazimu waziri Kagwe kutumia gari rasmi la serikali kusafiri kurejea Nairobi kufuatia hitilafu kwenye ndege hiyo.
Kagwe alikuwa amezuru kaunti ya Kericho kukagua namna hospitali katika kaunti hiyo zimejiandaa kukabiliana na msambao wa virusi vya corona.