Mji mkuu wa Kenya, Nairobi, umeorodheshwa miongoni mwa miji minane bora vilivyona utajiri barani Afrika, ukilenga wawekezaji katika sekta za teknolojia, usimamizi wa mali na bidhaa mbalimbali.
Ripoti ya ‘Centi-millionaire Report 2024’ iliyotolewa na kampuni YA Henley and Partners inaiweka Nairobi katika nafasi ya nane barani na 65 kimataifa kwa miji ya kutazamwa kutokana na ukuaji na maendeleo yake ya haraka.
“Sekta ya teknolojia inakuza uzalishaji wa haraka wa utajiri jijini Nairobi, huku jiji hilo sasa likiwa mwenyeji wa mamilionea 10 kati ya 342 barani Afrika,” Juerg Steffen, Mkurugenzi Mtendaji wa Henley & Partners amesema.
Pia inataja kuongezeka kwa maendeleo ya hali ya juu katika maeneo kama Upper Hill na Westlands kutokana na mahitaji yanayoongezeka kutoka kwa mabwenyenye.
“Maboresho haya yameundwa kuvutia watu binafsi wenye thamani ya juu na biashara za kimataifa, na kuongeza kasi ya ukuaji.”
Mji mkuu wa Misri- Kairo unaongoza barani Afrika ukifuatiwa na miji ya Afrika Kusini ya Cape Town na Johannesburg.
Hivi sasa ripoti hiyo inaonyesha kuwa kuna watu 29,350 ulimwenguni kote waliowekeza mali yenye thamani ya dola milioni 100 au zaidi.
Mataifa ya Uchina na Marekani ndiyo yanaoongoza kwa idadi kubwa ya mabwenyenye wenye thamani kubwa ulimwenguni.