Mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma Nordin Haji ametoa kibali cha kushtakiwa kwa naibu chansela wa chuo kikuu cha Maasai Mara Mary Walingo kuhusiana na wizi wa shilingi million 177.
Katika taarifa, Haji anasema kuna ushahidi wa kutosha kudhibitisha kuwa kati ya mwaka 2016-2019, mamilion ya pesa yaliyotolewa kwenye akaunti za chuo hicho na kutumika kwa shughuli za kibinafsi.
Wengine ambao Haji amependekeza wafunguliwe mashtaka kuhusiana na sakata hiyo ni makamu wa naibu chansela wa fedha Profesa Simon Kasaine, kaimu naibu chansela wa masomo na masuala ya wanafunzi Profesa John Almadi Obere, afisa wa fedha Anaclet Biket Okumu na dereva wa Walingo Noor Hassan Abdi.
Watano hao huenda wakatiwa mbaroni hii leo kuhojiwa na makachero kutoka tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC kwa ushirikiano na wale kutoka idara ya upelelezi DCI kabla yao kufunguliwa mashtaka.









