Mwangangi ateuliwa afisa mkuu mtendaji wa SHA

0
Daktari Mercy Mwangangi (katika hafla ya awali.)

Katibu msaidizi (CAS) wa zamani katika wizara ya afya Dr. Mercy Mwangangi ameteuliwa kuwa afisa mkuu mtendaji wa mamlaka ya afya ya jamii (SHA).

Uteuzi wa Mwangangi aliyehudumu wakati wa utawala wa rais mstaafu Uhuru Kenyatta ulitangazwa kupitia taarifa iliyotolewa na waziri wa afya Aden Duale siku ya Ijumaa.

“Wizara inampongeza Daktari Mwangangi kwa kuteuliwa kwake na inamtakia mema anapokuwa afisa mkuu mtendaji wa kwanza wa mamlaka ya afya ya jamii (SHA). Tuna uhakika kwamba ana tajriba hitajika kuongoza SHA na pia kutekeleza majukumu aliyotwikwa,” Duale alisema.

Wizara hiyo aidha ilitaja kuwa uteuzi wake ulitokana na uzoefu wa miaka mingi katika sekta ya afya ambao ulitarajiwa kumwezesha kusaidia katika utekelezaji wa mamlaka ya afya ambayo imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali.

Kuteuliwa kwa Mwangangi kunafuatia kukamilika kwa mchakato wa kumsaka ambaye angejaza nafasi hiyo iliyokuwa imemezewa mate na wakenya 92 ambao walikuwa wametuma maombi.

Hata hivyo Mwangangi alifaulu kuwa miongoni mwa wawaniaji kumi na wawili waliorodheshwa na kuhojiwa ili kutwaa wadhifa huo.

Daktari Mwangangi ambaye amekuwa mkurugenzi mkuu wa uimarishaji wa mifumo ya afya katika shirika la utafiti wa kimatibabu barani Afrika (Amref) atakuwa akichukua nafasi ya Robert Ingasira aliyekuwa akishikilia nafasi ya afisa mkuu mtendaji wa SHA kikaimu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here