Rais William Ruto amewasihi Wakenya kushiriki katika ukosoaji wa maana unaozingatia ukweli hata wanapopinga sera na miradi inayotekelezwa na utawala wake.
Rais Ruto, ambaye alikuwa akizungumza wakati wa sherehe za Jamhuri Day pia ameonya kuwa nchi inaweza kutumbukia shimoni ikiwa Wakenya watatilia shaka kila ajenda ya maendeleo.
Mkuu wa Nchi amewakumbusha Wakenya kwamba mafanikio ya kidemokrasia na ajenda ya maendeleo ya nchi iko hatarini kwa ukosoaji wa mara kwa mara ambao msingi wake ni uwongo.
“Kwa hivyo ninawaomba Wakenya wote kushiriki kikamilifu katika mazungumzo yetu ya kidemokrasia, hata tunapofanya kazi kwa bidii katika ujenzi wa taifa. Wakati wote, na tujitahidi kujihusisha kwa msingi wa ukweli,” amesema kiongozi wa taifa .
Rais amesisitiza kuwa serikali yake imesajili mafanikio makubwa ila anapondwa mitandaoni pasi na watesi wake kuzingatia hali halisia.
“Tunaposema kwamba gharama ya bidhaa za msingi za chakula imeshuka, ni ukweli. Tunaposema mfumuko wa bei umepungua, ni ukweli,” Ruto amesema.
“Tunaposema kwamba wakulima wetu wanazalisha zaidi na kwa njia bora, ni ukweli, na tunaposema kwamba Wakenya ambao wamejiandikisha kwa Taifa Care wanapokea huduma bora kuliko hapo awali, ni ukweli.” Ameongeza Rais.
Wakati uo huo, rais ametoa onyo kwa wakosoaji akisema hivi karibuni watakosa maneno ya kusema wakati miradi mingi ya maendeleo itakapoanza kuzaa matunda.
“Watasema nini katika mwezi ujao tutakapoanza kutoa funguo kwa wamiliki wapya wa nyumba za bei nafuu? Watasemaje kuhusu maelfu ya mafundi, walimu, wahudumu wa afya, wafanyakazi wa majengo na ujenzi, wafanyakazi wa kidijitali na wengine wengi ambao tayari wapo kazini, wakiwemo vijana 300 wa kike na wa kiume walioagizwa na makamu wangu kufanya kazi nje ya nchi.?”