Kinara wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi amemshauri rais Uhuru Kenyatta kufanya mashauriano ya kina kabla ya kutoa uamuzi kuhusu hatma ya kulivunja bunge alivyoshauriwa na jaji mkuu David Maraga.
Mudavadi katika taarifa ameonya kuwa taifa hili litatumbukia kwenye mgogoro wa kikatiba iwapo swala hilo halitashughulikiwa kwa umakini unaostahili.
Ameongeza kuwa bunge linatekeleza jukumu muhimu katika uongozi wa taifa na hivyo kulivunja na kuwatuma wabunge nyumbani kwa kushindwa kujadili na kupitisha sheria kuhusu usawa itakuwa ni kukaribisha mgogoro wakati ambapo taifa hili linakumbwa na janga la corona ambalo limeyumbisha uchumi.









