Kupungua kwa maambukizi mapya ya virusi vya corona nchini hakumaanishi kwamba masharti ya usalama yanafaa kulegezwa.
Ndio wito unaotolewa kwa Wakenya na kaimu mkurugenzi wa huduma za matibabu katika wizara ya afya Dkt. Patrick Amoth ambaye anasisitiza kuwa ugonjwa huo ungali unasambaa.
Na licha ya maambukizi mapya kupungua kutoka asilimia 13% mnamo mwezi Julai mwaka huu na kufikia asilimia 7% kwa sasa, Dkt. Amoth anamshauri kila mkenya kuendelea kuzingatia masharti ya usalama ikiwemo kuvalia barakoa, kuepuka mikusanyiko ya watu sawa na kudumisha usafi wa hali ya juu.
Idadi ya visa vya ugonjwa huo nchini kwa sasa ni 34,315 baada ya kupima sampuli 456,088, idadi ya waliopona ni 20,211 huku maafa yanayotokana na ugonjwa huo yakiwa 577 kati yao wakiwa wanaume 432 na wanawake 145.