MSHUKIWA WA MAUAJI YA AFISA WA WELLS FARGO KUENDELEA KUZUILIWA

0

Bunduki ya kibinafsi iliyokuwa ikimilikiwa na Meneja katika kampuni ya Wells Fargo aliyeuwawa imepatikana.

Maafisa wa DCI katika ukanda wa Nyanza aidha wamewakamata wanawake wawili ambao ni washukiwa wa mauji ya Willis Ayieko huku mshukiwa wa tatu akifanikiwa kukwepa mtego wa polisi.

Mshirikishi wa DCI Lenny Kisaka amesema kuwa walipata ripoti ya jaribio la wizi katika Barabara ya Lwanda na kuweka mtego ambapo walitia mbaroni wawili hao.

Hata hivyo mmoja wa washukiwa alifanikiwa kukwepa mtego huo na kutoroka.

Hayo yanajiri wakati ambapo mahakama imeruhusu Victor Okot Ouma mshukiwa mkuu wa mauaji hayo kuzuiliwa kwa siku 21 katika kituo cha Polisi cha Railways jijini Kisumu.

Hakimu Jacob Mkala wa mahakama ya Siaya ameagiza Okoth kufanyiwa uchunguzi wa kiakili kabla ya kurejeshwa mahakamani.

Kwa mujibu wa Polisi, Okoth alinaswa kwenye kanda ya video ya siri CCTV akiwa katika eneo ambapo gari la Willis Ayieko aliyekuwa meneja katika kampuni ya Wells Fargo ilipatikana.

Ripoti ya uchunguzi wa maiti ya mwendazake uliofanywa jana ulifichua kuwa aliaga kutokana na kufuja damu kutokana na jeraha kichwani.

Mwanapatholojia Mkuu wa serikali Johansen Oduor aidha alifafanua kuwa sehemu za mwili wa Ayieko zilinyofolewa huku baadhi zikiliwa na ndege wa mwituni.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here