Erick Mutinda, mshukiwa wa mauaji ya mwanafunzi mwenzake wa chuo kikuu cha Multimedia (MMU) atazuiliwa kwa siku 21 ili kuwezesha polisi kukamilisha uchunguzi.
Mutinda alikamatwa Ijumaa katika eneo la Sultan Hamud kufuatia kupatikana kwa mwili wa Sylvia Kemunto ndani ya tangi la maji lililokuwa juu ya jengo la shule.
Mawakili wa familia ya mwendazake wakiongozwa na Danstan Omari waliiambia mahakama Jumatatu kuwa familia hiyo ilikuwa imeathirika mno kutokana na mauaji ya mpendwa wao wakilitaja tukio hilo kuwa mauaji yaliyolenga jinsia ya kike.
“Kosa linadaiwa kutekelezwa katika chuo cha Multimedia, taasisi ambapo kila mzazi humtuma binti wao akiamini kuwa ni pahali salama.” Wakili Omari aliiambia mahakama.
Hata hivyo upande wa utetezi uliiambia mahakama kuwa mshukiwa mwenye umri wa miaka 19 alikuwa tayari kushirikiana kikamilifu katika uchunguzi.
Ikiridhia ombi la upande wa mashtaka la kumzuilia mshukiwa, mahakama ya Kibera ilikiri uzito wa kesi hiyo na kusisitiza umuhimu wa kuwapa maafisa wa upelelezi muda wa kutosha utakaowawezesha kukamilisha uchunguzi.
Kutokana na uchunguzi wa awali mahakama iliambiwa kuwa Kemunto, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza aliyekuwa akisomea kozi ya uwanahabari na Sayanzi ya Kompyuta alikuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na mshukiwa aliyekuwa akisomea Uhandisi wa Umeme tangu Septemba mwaka wa 2024.
Mutinda atazuiliwa katika kituo cha polisi cha Capitol Hill kesi hiyo ikiratibiwa kutajwa tarehe 24 Aprili.