Mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Harambee Stars Anthony “Teddy” Akumu ana uhakika kuwa Timu hiyo itafuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika 2025 nchini Morocco.
Hii ni licha ya kujumuishwa katika Kundi gumu la ‘J’ pamoja na Zimbabwe, Namibia na Cameroon.
Mchezaji huyo wa zamani wa Gor Mahia na Orlando Pirates anaamini kuwa Stars ina kikosi imara kutoa ushindani na kujikatia tiketi ya kushiriki kinyang’anyiro cha Afcon. Stars itamenyana na Zimbabwe Septemba tarehe 6, 2024, katika mechi ya ufunguzi mjini Kampala, Uganda, kabla ya kumenyana na Malawi nchini Afrika Kusini Septemba 10.
Akumu alikosa kushiriki michuano ya mwaka wa 2019 nchini Misri chini ya kocha wa wakati huo Sebastian Migne lakini anaamini kwamba atakuwa na mchango muhimu kwa kikosi cha Stars.
Akumu hata hivyo amekubali kuwa wana Harambee Stars wana kibarua kigumu kilicho mbele yao akisistiza kuwa watajitahidi angalau kunyakua tikiti moja kati ya mbili za kwenda Rabat, Morocco kushiriki Ubingwa wa Afrika.
Licha ya kuwa bila klabu kwa muda wa miezi saba, Akumu alikuwa na mchango mkubwa wakati Stars ilipotwaa Kombe la Mataifa Nne kwenye Uwanja wa Taifa wa Bingu nchini Malawi. Akumu vile vile alionyesha mchezo mzuri wakati Kenya ilipomenyana na Burundi na Ivory Coast katika mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia Kocha Mkuu wa Stars, Engin Firat akisifia mchezo wake.
Kocha Firat alimtetea Akumu akisema yuko fiti kuliko wachezaji wengi wa Ligi Kuu ya Kenya, anafanya kazi kwa bidii na anaendana na mfumo wake.
Akumu alitemwa na wababe wa Afrika Kusini, Kaizer Chiefs mnamo Julai 2, 2022. Alijiunga na Sagan Tosu ya Japan mnamo Desemba 2023, ambapo alicheza mechi tatu pekee za Kombe la Ligi kabla ya kusitisha huduma zake mwezi Januari 10, 2024. Kwa sasa anahusishwa na upande wa Iran Kheybar Khorramabad, ambapo alitia saini nao Julai 7.