Kamati ya bunge la Senate inayoangazia namna serikali inavyoshughulikia janga la COVID19 imemuagiza mkaguzi mkuu wa hesabu za umma kufanya ukaguzi katika kaunti zote 47 kubaini namna serikali hizo zimetumia pesa zilizotengwa kukabiliana na janga hilo.
Ukaguzi huo unaotarajiwa kufanyika chini ya mwezi mmoja ujao utaanzia mwezi Machi wakati kisa cha kwanza cha corona kiliposhuhudiwa nchini hadi Julai 31.
Kuu kwenye ukaguzi huo ni kiasi cha pesa ambacho kila kaunti ilipokea kwa minajili ya kukabiliana na janga hilo na jinsi zilivyotumika kuafikia lengo hilo.
Mkaguzi mkuu wa hesabu za umma anatarajiwa kuifahamisha kamati hiyo iwapo kulikuwa na wizi wowote au pesa hizo kutumika visivyo pasipo kuzingatia kanuni zilizopo.