MGOMO WA WAFANYIKAZI WAKWAMISHA SHUGHULI KWENYE UWANJA WA NDEGE WA JKIA, MOI ELDORET

0

Shughuli za Usafiri zimetatizika katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta JKIA na uwanja wa Ndege wa Moi Eldoret mgomo wa wafanyikazi wa viwanja hivyo vya ndege viking’oa nanga hii leo.

Kampuni mbili kuu za usafiri wa angani Kenya Airways na Fly540 zimesema zimelazimika kukatiza safari zao ndani na nje ya nchi kutokana na mgomo huo.

Wafanyikazi hao kupitia muungano wao wa KAWU wanataka kufutiliwa mbali kwa kandarasi kati ya Serikali na kampuni ya India ya Adani ambapo kampuni hio inatarajiwa kutwishwa jukumu la usimamizi wa uwanja huo kwa maika 30.

“Hatutarejea kazini hadi pale tutakapoangamiza zimwi hili la Adani,” amesema katibu mkuu wa KAWU Moss Ndiema.

Wasafiri wengi katika uwanja wa JKIA wametatizika baada ya safari zao kukosa kung’oa nanga kwa wakati ulioratibiwa.

Waliozungumza na meza ya shajara wameelezea kutamaushwa na hali hio wakitaka hatua za haraka kuchukuliwa kurejesha hali ya kawaida katika uwanja huo mkubwa zaidi katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

“ Nilikuwa nisafiri kusaka matibabu lakini sasa nimekwama. Sijui kama nitafika niendako na kuhudumiwa,” amesema Mugisha Christian ambae ni Raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Vurugu imeshuhudiwa wakati maafisa wa polisi walipojaribu kukabili wafanyikazi hao.

Baadhi ya wafanyikazi wa uwnaja huo na wakuu wa muungano wao wametiwa mbaroni kutokana na vurugu hivyo.

Iwapo kandarasi hio itaendelea Kampuni ya Adani inatarajiwa kuboresha uwanja wa JKIA kwa kujenga kituo kipya cha kupokea wasafiri, kujenga anga tua mpya ambapo itakuwa ni mara ya kwanza kwa uboreshaji wa aina hio kufanywa kwa miaka 40.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here