Baraza kuu la vyombo vya habari nchini MCK limekosoa kufukuzwa kwa wanahabari kwenye vikao vya kumhoji waziri wa usalama wa ndani Dkt. Fred Matiang’i na Inspekta mkuu wa Polisi Hillary Mutyambai kuhusu kukamatwa kwa maseneta watatu.
MCK kupitia taarifa iliyotumwa na afisa mkuu mtendaji David Omwoyo imesema kufukuzwa kwa wanahabari na kamati inayoongozwa na seneta wa Garissa Yusuf Hajji haitakubalika kamwe chini ya katiba kwani waandishi wa habari walikuwa wanawajibikia majukumu yao ya kikatiba kutafuta taarifa kuwajuza wananchi.
Maseneta Kipchumba Murkomen wa Elgeyo Marakwet na mwenzake wa Makueni Mutula Kilonzo Jr vile vile wamekosoa hatua hiyo wakihoji kwamba Wakenya wana haki ya kufahamu ukweli kuhusiana na kutiwa mbaroni kwa wenzao watatu siku ya Jumatatu.
Maseneta hao Cleophas Malala wa Kakamega, Steve Lelegwe Samburu na Christopher Langat wa Bomet waliachiliwa huru baada ya kuhojiwa bila kushtakiwa.