Mchakato wa kumng’oa gavana wa Migori Okoth Obado unaanza Jumanne hii huku kiongozi wa wengi katika bunge la kaunti hiyo Ken Ouma akitazamiwa kuwasilisha notisi ya kulifahamisha bunge kuhusu hoja ya kumuondoa gavana huyo.
Ouma ambaye anazingatia uamuzi ulioafikiwa kufuatia mkutano wa chama cha ODM anasema mchakato huo utaendelea licha ya kuwepo kwa madai ya baadhi ya wawakilishi wadi kutishiwa maisha.
Mchakato huo utampa nafasi spika wa bunge la kaunti hiyo kuratibu tarehe ya kujadiliwa kwa hoja hiyo ambapo gavana Obado aliyeshtakiwa kwa ufisadi atapewa nafasi ya kujitetea.
Haya yanajiri huku baraza kuu la vijana kutoka kaunti hiyo ya Migori likiongozwa na Julius Omamba likitaka mchakato wa kumumbandua Obado kuharakishwa ili kuondoa hali ya sintofahamu inayowakumba wakaazi wa kaunti hiyo.