Baada ya zaidi ya mwongo mmoja wa sintofahamu na kubadilisha jina la sikukuu ya kitaifa ya tarehe 10 mwezi Oktoba nchini Kenya, ‘Mazingira Day’ imeadhimishwa nchini kwa mara ya kwanza.
Hapo awali, siku hii ilijulikana kama ‘Moi day’, iliyotoa nafasi ya kuangazia mafanikio ya rais wa pili wa Kenya Daniel arap Moi, ambaye alichukua mamlaka baada ya kifo cha rais wa kwanza Mzee Jomo Kenyatta, Agosti 1978.
Hata hivyo, hadhi ya Moi day kama sikukuu ya kitaifa ilikabiliwa na hatma isiyojulikana baada ya taifa kupata katiba mpya Agosti 2010, na kusababisha kupoteza nafasi yake miongoni mwa orodha ya sikukuu za kitaifa nchini.
Kwa miaka saba, siku hii kama ilivyojulikana wakati huo ilifutika kwenye kalenda ya taifa kabla hali kubadilika mnamo 2017 uamuzi wa Mahakama ya Juu ulipoirejesha Jaji George Odunga akisema ubatilishaji huo ulikuwa ukiukaji wa sheria ya sikukuu za kitaifa.
Jaji Odunga alibainisha kuwa kama bunge lilikuwa na maoni kwamba siku ya Moi haikupaswa kuendelea kuzingatiwa kama sikukuu, lilipaswa kurekebisha sheria ipasavyo.
“Natoa tamko kwamba kuachwa kwa siku ya Oktoba 10 kuadhimishwa kama sikukuu ni kinyume cha sheria na ni kinyume cha Kifungu cha 2(1) kama kilivyosomwa na sehemu ya kwanza ya Sheria ya Sikukuu za Umma,” alisema Odunga.
“Isipokuwa hadi bunge lirekebishe Sheria husika au waziri abadilishe tarehe nyingine, tarehe 10 Oktoba kila mwaka itaendelea kuwa sikukuu,” Jaji alisema.
Uamuzi huo ulifuatia kesi iliyowasilishwa na Gregory Nyauchi dhidi ya mawaziri wa Mambo ya Ndani, Jumuiya ya Afrika Mashariki, leba na mwanasheria mkuu wa serikali.
Nyauchi alikuwa amepinga kuondolewa kwa likizo hiyo akisema kulikuwa na athari kubwa ambayo ingezuia wafanyikazi kupokea marupurupu yao kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Ajira.
“Tunaishi katika nchi ambayo ni wachache tu wanapewa siku 21 za likizo ambazo Sheria ya Ajira inaruhusu. Watu wengi huamka na kwenda kazini kila siku isipokuwa wikendi. Katika nchi yenye mtazamo hasi kuhusu haki za wafanyakazi kama ile inayoonyeshwa na wengi wa waajiri wetu, likizo ya umma ni jambo la lazima,” Nyauchi alisema wakati huo.
Aidha, alidai kuwa wakenya wote wako sawa mbele ya sheria, na kama ilivyokuwa kwa rais wa kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta, mrithi wake Moi alistahili siku iliyotajwa kwa heshima yake.
Siku ya Moi iliadhimishwa mwaka uliofuata wa 2018 bila juhudi nyingi za serikali.
Mnamo Desemba 2019, Baraza la Mawaziri likiongozwa na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, liliidhinisha kubadilisha jina siku hiyo kuwa Siku ya Huduma, ikionyesha mwito wa rais wa zamani Daniel arap Moi, ambaye aliiona kama siku maalum ya ‘huduma na kujitolea’.
Mwaka mmoja baadaye, sikukuu hiyo iliyoadhimishwa Oktoba 10 ilifanyiwa mabadiliko mengine kwani ‘Huduma’ ilitoa nafasi kwa Siku ya ‘Utamaduni’, ambayo ilitumiwa kuadhimisha utofauti wa tamaduni za Kenya na kutoa jukwaa kwa wakenya kuthamini zaidi ya makabila 44 nchini.
Miezi mitano iliyopita, siku hiyo ilibadilishwa tena jina na kuwa siku ya Mazingira baada ya rais William Ruto kuidhinisha Mswada wa Marekebisho ya sheria wa 2024.
Hatua hii inaendana na msukumo wa serikali wa kufanikisha mpango wa miaka 10 wa upandaji miti bilioni 15 unaojumuisha urejeshaji wa misitu katika juhudi za kuhifadhi mazingira.