Spika wa bunge la Senate Ken Lusaka ameitisha kikao kingine maalum Jumatatu ijayo kujadili mswada tata wa ugavi wa mapato.
Lusaka katika notisi amesema kibarua cha kipekee siku hiyo itakuwa ni kuwapa maseneta nafasi ya kutanzua mgogoro uliopo kuhusu mfumo unaopaswa kutumiwa kugawa fedha katika serikali za kaunti.
Kikao hicho kinatazamiwa kuandaliwa saa nne asubuhi na kisha bunge kuelekea kwenye likizo hadi Septemba 8 kulingana na kalenda ya bunge la Senate.
Itakumbukwa kwamba juhudi za mwanzo kujaribu kutanzua kitendawili hicho kuhusu ugavi wa pesa kwenye kaunti zimeambulia patupu huku maseneta wakishindwa kuelewana na kulazimu vikao kuhusu mjadala huo kuhairishwa.