Mambo bado kwa gavana Obado

0

Mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma Noordin Hajji ameidhinisha kukamatwa na kushtakiwa kwa gavana wa Migori Zachary Okoth Obado pamoja na wanawe wanne kuhusiana na sakata ya wizi wa Sh73M pesa za kaunti hiyo.

DPP katika taarifa amesema uchunguzi umebaini kuwa kampuni zinazohusishwa na watoto wa gavana huyo zililipwa pesa na kaunti hiyo kipindi cha matumizi ya pesa mwaka 2013/2014 na 2016/2017.

Watoto wa gavana huyo wanaohusishwa na sakata hiyo ni Dan Okoth, Susan Okoth, Jerry Okoth na Adhiambo Okoth.

Uchunguzi wa DPP umebaini kuwa Sh38M zilitumwa kwenye akaunti za benki za wanawe watatu kulipia karo na pesa za matumizi wakiwa nchini Australia, Scotland na Uingereza.

Pesa hizo zilizoibwa aidha zimepatikana kuwa zilitumika kununua magari aina ya Toyota na Land Cruicer V8.

Sh34M zinadaiwa kutumika katika ununuzi wa nyumba ya kifahari mtaani Loresho Ridge jijini Nairobi mmiliki wake akiwa ni bintiye gavana Obado, Evelyne Adhiambo Zachary.

EACC inasema washukiwa watashtakiwa kwa mashtaka manne ikiwemo kushirikiana kutekeleza ufisadi, ulanguzi wa pesa pamoja na unyakuzi wa mali ya umma.

Obado na wenzake wana Jumatano asubuhi kujasalimisha katika afisi za EACC.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here